HISTORIA FUPI YA KANISA LA EAGT
![]() |
![]() |
|
| Mch. Dkt. Brown Mwakipesile Askofu Mkuu wa Saa wa EAGT |
Mch. Dkt. Moses Kulola Askofu Mkuu wa Kwanza wa EAGT |
Kanisa la “The Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT)” lilisajiliwa rasmi na Wizara ya Mambo ya Ndani (Dar es Salaam, Tanzania), tarehe 18 Julai 1991. Muasisi Mkuu wa dhehebu hili alikuwa Mwinjilisti Dkt. Moses Samuel Kulola (Hayati), pamoja na Watumishi wengine wa Mungu waliokuwa na moto wa Injili ndani yao na mzigo wa kuona Injili ya kweli inahubiriwa kwa nguvu ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Uongozi wa kwanza wa kitaifa wa Kanisa la EAGT ulikuwa kama ifuatavyo: Askofu Mkuu – Mwinjilisti Moses Kulola; Makamu Askofu Mkuu – Mchungaji Moses Mwamwenda; Katibu Mkuu na Mweka Hazina Mkuu – Mchungaji Mark Mhina; na Mshauri Mkuu – Mchungaji Anyandwile Mwakisyala. Vilevile, ziliundwa Kanda nne (4) na uongozi wake ukawekwa kama ifuatavyo: Kanda ya Kaskazini – Mchungaji Samuel Mwaliego; Kanda ya Magharibi – Mchungaji John Mahene; Kanda ya Mashariki Kusini – Mchungaji Ahmed Makajula; na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini – Mchungaji Asumwisye Mwaisabila.
Baada ya Kanisa la EAGT kusajiliwa, kazi ya Injili iliendelea kwa kasi na EAGT ikafungua makanisa kwa wingi. Hata hivyo, katika nyakati za mwanzo za Kanisa la EAGT, kulikuwa na changamoto ya kutokuwa na nyumba rasmi za ibada, jambo lililosababisha makanisa mengi ya EAGT kuanza kuabudia katika madarasa ya shule, nyumba za watu binafsi, kumbi mbalimbali na hata chini ya miti. Katika kipindi hicho cha mpito, EAGT iliomba vibali Halmashauri za miji na wilaya kuruhusu madarasa ya shule kutumiwa kama vyumba vya ibada, na tunaishukuru Serikali kwa kutoa kibali kwa wakati huo.
Kwa kuwa hatua ya kutumia madarasa ya shule kama vyumba vya ibada ilikuwa ni ya kipindi cha mpito tu, EAGT ililazamika kujenga makanisa kwa wingi na kwa kasi. Chini ya uongozi mahiri wa Askofu Dkt. Moses Kulola, ambaye alitwaliwa na Bwana tarehe 29 Agosti 2013, kazi hii ilifanyika kwa mafanikio makubwa. Baada ya Askofu Kulola kutwaliwa na Bwana, Mungu alimuinua Mchungaji Dkt. Brown Abel Mwakipesile kuwa Askofu Mkuu wa Pili wa Kanisa la EAGT, na akaiendeleza kazi hii kwa kasi zaidi. Tunamshukuru Mungu kwamba sasa tuna makanisa zaidi ya 6,000 yaliyoenea mikoa na wilaya zote nchini Tanzania, na hata nje ya Tanzania. Hata hivyo, EAGT inaona kwamba bado makanisa haya hayatoshi kwani kuna baadhi ya maeneo hayajafikiwa kikamilifu ukilinganisha na uhitaji uliopo. Kwa sababu hiyo, dhamira ya EAGT ni kuendelea kuhubiri Injili kwa nguvu, kujenga makanisa mengi zaidi, na kuwafikia watu wote.
Pamoja na changamoto nyingi ambazo Kanisa la EAGT imekumbana nazo tangu kuanzishwa kwake, Mungu amekuwa mwaminifu sana na ameendelea kulikuza na kuliimarisha Kanisa hili. Yako mafanikio mengi ya kumshukuru Mungu na ya kujivunia, ukilinganisha na mwanzo ulivyokuwa mgumu. Tangu usajili mwaka 1991, EAGT imeenea mikoa yote na wilaya zote, ina miradi ya kitaifa, Shule za Sekondari, Vyuo vya Theolojia, televisheni, redio na mambo mengine mengi mazuri. Hadi mwaka 2025, EAGT ilikuwa na kanda 13 kutoka kanda 4 wakati EAGT inaanza, na majimbo 103 kutoka majimbo 15. Kanisa la EAGT limejikita kwenye sera ya utakatifu na kumtafuta Mungu kwa moyo wote, na linaamini kwamba hili ni jambo muhimu kuliko mambo mengine yote.

